Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umetaja mambo
nane yatakayosababisha Kura ya Maoni isipigwe Aprili 30 kama
ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete, licha ya kazi ya kuandikisha
wananchi kwenye Daftari la Wapigakura kuendelea mkoani Njombe.
Kazi hiyo ya uandikishaji wapigakura ambayo ni
muhimu katika mchakato wa Kura ya Maoni ya kupitisha au kukataa Katiba
Inayopendekezwa, imekuwa na changamoto nyingi kutokana na kutumia
teknolojia ya ‘Biometric Voters Registration’ ambayo hukusanya taarifa
za mpigakura, ikiwa ni pamoja na alama za vidole.
Ukawa, ambayo inaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi,
Chadema, CUF na NLD, pia imetaka fedha ambazo zimetengwa na Serikali kwa
ajili ya Kura ya Maoni, kupelekwa kwenye uboreshaji wa Daftari la
Wapigakura kwa maelezo kuwa uboreshaji unaondelea mkoani Njombe
unakabiliwa na changamoto nyingi na kutaka kura ya Maoni kuahirishwa
hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo imekuja siku tatu baada ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuanza kuandikisha wakazi wa mji mdogo wa
Makambako, ambapo kwa kasoro hizo wakazi wake wamelazimika kuiomba Nec
kuongeza maofisa na vitendea kazi ili kuwezesha shughuli hiyo kukamilika
ndani ya muda uliopangwa.
Viongozi wa Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema),
Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Dk Emmanuel Makaidi (NLD) na Mosena
Nyambabe (NCCR-Mageuzi), walitoa kauli hiyo jana wakati wakizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakisisitiza kuwa Serikali
inalazimisha mambo isiyoyaweza.
Akitaja sababu hizo, Profesa Lipumba alisema:
“Kwanza, Nec haina watumishi wa kufanya kazi ya uandikishaji. Mshauri
mwelekezi kutoka Marekani aliishauri tume kuwa inahitaji kuwa na
watumishi 10,000 ili kufanikisha uandikishaji nchi nzima na wapewe
mafunzo ya kina ya kutumia mashine hizo.”
Alisema watumishi waliopo Makambako ni wachache na
wamepewa mafunzo ya siku moja tu, kabla ya kuanza kwa uandikishaji, na
wengi wao hawajui kutumia kompyuta wala kamera ambazo ndiyo zinazotumika
kuchukua taarifa muhimu.
Alitaja sababu ya pili kuwa ni Nec kukabiliwa na
uhaba wa fedha kwa maelezo kuwa ilipewa jukumu la kuboresha Daftari la
Wapigakura bila kutengewa fedha za kutosha za kununulia vifaa, kuajiri
na kuwapa mafunzo wafanyakazi husika sambamba na kutoa elimu kwa
wananchi.
“Tatu, Tume haisemi ukweli juu ya suala zima la
uandikishaji. Wamesema watakamilisha kazi Aprili 28 na 30 itafanyika
Kura ya Maoni. Nchi ina watu milioni 24 wenye haki ya kupiga kura na
haiwezekani wakaandikishwa kwa muda uliobaki,” alisema.
Alisema sababu ya nne ni mashine za BVR kuwa na
kasoro nyingi, ikiwamo ya kutotambua alama za vidole gumba vya wananchi
ambao wanafanya kazi ngumu, hivyo vidole vyao kuwa na sugu ambao wengi
wao ni wakulima, wafugaji na wachimbaji wa madini.
“Sababu ya tano, ni Nec kupuuza ushauri wa mshauri
mwelekezi ambaye aliitahadharisha tume hiyo kwamba haiwezekani kutumia
mfumo wa BVR kukamilisha kazi kwa wakati kutokana na changamoto
zinazoikabili tume hiyo, ikiwamo ya ukosefu wa fedha, uchache wa
watumishi, ” alisema.
Akizungumza na Mwananchi mapema wiki hii,
mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alisema ushauri wa mtaalamu huyo
ni wa siku nyingi na kwamba alitaka utumike mfumo wa zamani, lakini tume
yake imekataa.
No comments: